Manusura wa ugonjwa hatari wa saratani kutoa ombi kwa serikali ya Jimbo la Makueni kukabiliana vilivyo na uenezaji wa ugonjwa huo.Waliyasema hayo walipokuwa wamejumuika pamoja katika hospitali ya serikali ya Makindu hapo jana Jumamosi tarehe 3 Januari,2018.
Walifurahia kutibiwa na kupona ugonjwa huu hatari chini ya jua ambao unasemekana kuwa umeangamiza watu wengi.Hawakusahau kulalamikia kiasi kikubwa cha fedha kinachohitajika ili mgonjwa apate matibabu dhidi ya ugonjwa huo.Walishauri serikali ya gatuzi la Makueni kushirikiana kikamilifu na serikali kuu ya kitaifa inayoongozwa na Mtukufu Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Mtukufu William Samoei Ruto ili kufanikisha huduma za matibabu ya kansa.
Manusura hao waliongeza kwamba wengi wao hulazimika kuuza mashamba yao ili angalau kupata kiasi fulani cha pesa kuwawezesha kugharimu mahitaji ya matibabu.Serikali zote za mashinani zinastahili kuwajibikia afya njema kwa wakaazi wake ili kuwezesha kiwango cha juu cha maisha kupatikana.
Kwa pamoja waliunda kundi chao ambacho watakitumia kuhamasisha wakaazi wa Kaunti ya Makueni na Kenya kwa jumla kuhusu kuwepo haja ya kujitokeza kwa wingi na kupata kupimwa ugonwa wa kansa.Kwa kila wanawake 100,000 imebainika kwamba 34 huwa na saratani ilhali kwa wanaume 100,000 ni 17 ambao huwa na ugonjwa huo.Saratani ya matiti na nyungu ya mtoto imekuwa sugu kwa akina mama ilhali kwa wanaume kansa ya mishipa ya uzazi imekuwa ikikithiri jinsi wakati unavyoenda.
Walilalamikia kupiga foleni kwa muda wa hadi siku 3 katika hospitali kuu ya kitaifa hapa nchini Kenya na Jumuia ya Afrika Mashariki ya Kenyatta jijini Nairobi ili kupata huduma za matibabu.Huwa inawalazimu kutumia kiasi kikubwa cha fedha ili kupata matibabu dhidi ya jinamizi hili la ugonjwa wa maradhi ya mti almaarufu kansa.
Aidha,waliomba serikali ya gatuzi la Makueni kupitia wizara ya Afya na Usafi kujenga hospitali ya kushughulikia wagonjwa wa kansa ili kuwawezesha kupata matibabu karibu na kwa haraka.Hii ni kwa sababu wao hulazimika kusafiri hadi jijini Nairobi ili kupata dawa katika hospitali ya Kenyatta. Walisema kwamba wao hukumbana na changamoto zaidi baada ya kusafiri kwa mwendo mrefu huku wakitafuta matibabu.
Wakizungumza na Wanahabari katika Hospitali ya Kaunti- Ndogo ya Makindu,waliwarai wakaazi wa Makueni kuwa wakijitokeza kwa wakati unaofaa ili kupimwa ugonjwa huu ili wanaopatikana na ugonjwa huo wawe wakipata matibabu kuanzia wakati unaofaa kabla ya kusambaa kwake katika miili yao.
Mmoja wa Maafisa wa Afya Makueni Bi. Bretta Mutisya alisema kwamba ugonjwa wa kansa umeorodheshwa kuwa ugonjwa wa tatu hatari duniani kutokana na idadi kubwa ya watu ambayo umeangamiza.Afisa huyo aliongeza kwamba asilimia 60 ya Wakenya hupatwa na ugonjwa huo wakiwa chini ya umri wa miaka 70.
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Institute of Economic Affairs, ni wazi kwamba ifikapo mwaka wa 2026 kwa kila 100,000 kutakuwa na Wakenya 64 wa ugonjwa wa kansa kutokana na vilaji vya kisasa na mabadiliko katika hali ya maisha.